Idara hii inasimamia na kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa Sheria namba 8 ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 pamoja na Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003. Aidha, Idara ya Utawala na Utumishi inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya Utumishi wa Umma.
Idara hii imegawanyika katika makundi makuu mawili ambayo ni utawala na Utumishi.
Utawala
Wilaya ya Kyerwa ina Tarafa nne (4), Kata (24), Vijiji (99) na Vitongoji (668),aidha Wilaya inalo jimbo moja (1) la Uchaguzi ambalo ni Kyerwa likiwa na Mbunge mmoja wa Kuchaguliwa na Mbunge mmoja wa kuteuliwa.
Halmashauri ina madiwani 24 wa kuchaguliwa kutoka kila kata, na madiwani 8 wa viti maalumu. Kwa ujumla kuna madiwani 32 ikiwa ni pamoja na mheshimiwa mbunge 1 aliyepo katika jimbo la Kyerwa.
Kamati za kudumu
Halmashauri inaongozwa na kamati za kudumu tatu,ambazo pia maamuzi yake hujadiliwa na kuamuliwa na Baraza la madiwani.
Kamati ya Fedha,Uongozi,na Mipango
Kamati hii inaundwa na waheshimiwa madiwani pamoja na wakuu wa idara /vitengo wa Halmashauri.Mwenyekiti wa kamati hii pia ndiyo mwenyekiti wa Halmashauri,Mkurugenzi Mtendaji huwa ni katibu wa kikao.
Kamati hii hujadili na kutoa maamuzi/maazimio baada ya taarifa kujadiliwa kutoka kamati nyingine za kudumu na baadae kuziwasilisha katika Baraza la madiwani.Tofauti na kamati nyingine, kamati hii ina vikao vya robo(Kila baada ya miezi mitatu) na vikao vya kila mwezi ili kujadili mapato na matumizi.
Kamati ya Uchumi,Ujenzi,na Mazingira
Kamati hii hujadili na kutoa maamuzi taarifa zinazotoka katika idara ya mipango,ujenzi na zimamoto,ardhi na mazingira,na TEHAMA.Wajumbe wa kamati hii ni wataalamu wa Timu ya Menejimenti (CMT) na waheshimiwa Madiwani.
Kamati hii hukaa vikao vyake kila baada ya miezi mitatu isipokuwa kama kuna dharura .
Kamati ya Elimu,Afya na Maji
Kamati hii hujadili na kutoa maamuzi juu ya taarifa za utekelezaji wa idara ya Elimu Msingi na Sekondari,Idara ya Afya na Ustawi wa jamii,Maji, na Maendeleo ya jamii.
Wajumbe wa kamati hii ni wataalamu wa Timu ya Menejimenti(CMT) na waheshimiwa Madiwani.Kamati hii pia hukaa kikao kimoja kila baada ya miezi mitatu.
Mbali na kamati hizi kuna kamati nyingine mbalimbali katika Halmashauri kama vile kamati ya Ardhi na Mazingira, kamati ya UKIMWI, na kamati ya Maboresho.
Idara pia ina kitengo vya Usafirishaji chenye jukumu la kuratibu matengenezo/ukarabati wa magari na vyombo vingine vya moto. Pia kutoa vibali vya kutoka au kuingia gari katika himaya ya halmashauri,kudhibitisha utumiaji wa mafuta kwa vyombo vya moto kulingana na umbali gari litakaotembea.
Utumishi
Halmashauri ina watumishi wenye sifa na uweledi mkubwa wa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa manufaa ya taasisi na jamii. Hata hivyo ili kulinda ufanisi wa watumishi Idara imekuwa ikitoa mafunzo ya ndani na nje pale inapobidi kwa watumishi wa Halmashauri ili kuwajengea uwezo kupitia mpango wa mafunzo/masomoni wa kila mwaka wa fedha.
Aidha Halmashauri ina watumishi wanaofanya kazi Makao makuu ya Wilaya na watumishi ambao vituo vyao vya kazi ni katika kata.
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved