Mifugo na Uvuvi ni shughuli inayofanywa na wakazi wengi wa Wilaya ya kyerwa. Halmashauri kupitia Idara ya Mifugo na uvuvi imekuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha sekta hii inakuwa na matokeo chanya ya kuwainua kiuchumi Wavuvi na wafugaji waliotapakaa karibu Wilaya yote ya Kyerwa.
Kwa kuzingatia hili Halmashauri imeandaa andiko la mradi wa uwekezaji "District Investment Profile" katika sekta hii ambapo wawekezaji wanaweza kuja kuwekeza katika kuboresha thamani ya mazao yatokanayo na Mifugo na Uvuvi.
Miundombinu ya Mifugo iliyopo Wilayani
Majosho: Halmashauri ina jumla ya majosho 8 katika Kata za Mabira, Kimuli, Murongo, Bugomora, Isingiro (mawili ambayo ni Siina, na Kanyina), na Nkwenda. Majosho haya yote yanahitaji ukarabati ili yaweze utumika kwa kuwa yana ubovu wa viwango tofauti.
Malambo: Halmashauri ina lambo moja tu la Kyerwa ambalo lilichimbwa na wananchi kwa nguvu yao. Lambo hili limejengwa katika Kijiji cha Kyerwa kupitia njia shirikishi ya Fursa na Vikwazo kwa maendeleo (O & OD) iliibua mradi huu. Hata hivyo mradi huu umebadilishwa baada ya sehemu iliyokuwa imepangwa kwa shughuli hiyo kutengwa kwa ajili ya ujenzi wa Makao Mkuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa.
Machinjio: Kwa sasa Wilaya haina machinjio kubwa na ya kisasa, bali kuna sehemu tano (Machinjio ndogo) za watu binafsi ambazo zinatumika kwa ajili ya uchinjaji (miamba). Hata hivyo halmashauri imekwisha ainisha eneo la Rubwera kwa wawekezaji kuja kuwekeza katika Ujenzi wa Machinjio ya kisasa.
Minada ya Mifugo: Kuna mnada mmoja wa awali katika kijiji ya Katera.Hata hivyo shughuli za biashara ya mnada wa mifugo zimefungwa kutokana na kuwepo kwa karantini yamlipuko wa ugonjwa wa Miguu na midomo (F.M.D) katika wilaya ya Kyerwa.
Vibanio: Kuna vibanio vitatu katika maeneo ya Businde, Katera, na Ruhita. Vibanio hivyo hutumika katika kuwadhibiti Ng'ombe wakati wa kutoa huduma mbalimbali za Mifugo kama vile chanjo, kukata pembe na n.k.
Magonjwa ya Mifugo
Magonjwa ya mifugo yanayoathiri mifugo katika Wilaya ya Kyerwa ni yale yaenezwayo na Kupe kama vile Ndigana kali, Ndigana baridi, na moyo maji. Vilevile kuna magonjwa yaenezwayo na Mbung'o kama vile ugonjwa wa miguu na midomo, pamoja na BQ. Dalili za ugonjwa wa mapafu ya ng'ombe (C.B.P.P) zimeonekana katika kata ya Kaisho na Isingiro.
Ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa miguu na midomo tarehe 27 Julai 2012 iliwekwa karantini dhidi ya ugonjwa wa miguu na midomo. Eneo lote la Wilaya ya Kyerwa limeathirika.
Chanjo ya kuzuia Magonjwa ya Mifugo
Katika suala zima la kuzuia na kujikinga na magonjwa ya Mifugo, Chanjo mbalimbali za mifugo hutolewa na idara ya Mifugo na Uvuvi.
Pamoja na kuweka karantini, jitihada za kuzuia kuenea kwa maambukizi mapya ya ugonjwa wa miguu na midomo zinafanyika kwa kuwahamasisha wafugaji kuchanja Ng'ombe wao.
Uhimilishaji wa Mifugo
Hakuna shughuli za uhamilishaji zinazofanyika.Wafugaji wanahamasishwa ili kuibua mradi wa uhimilishaji wa mifugo ili kuboresha mifugo yao haraka na kuongeza tija na uzalishaji wa mifugo na mazao yake. Kwa kupitia mpango wa kilimo wa Wilaya (DADPs) uwezeshwaji utafanyika baada ya mpango huo kuibuliwa na wanufaika.Aidha, Wafugaji wanahamasishwa kuunda vikundi watakavyotumia kuchangia gharama kumpeleka kijana ambaye atagharamiwa ili kupata mafunzo juu ya uhimilishaji ili baadaye aje kutoa huduma hiyo kwenye maeneo ya wafugaji.
Uvuvi
Uvuvi ni mojawapo ya shughuli muhimu hapa Wilayani kwa kuwa yapo maziwa madogo yapatayo 7 na zipo jitihada za kuchimba malambo 4 ya kufugia samaki na kuzalisha vifaranga vya samaki.
Shughuli za uvunaji wa mazao ya Uvuvi Wilaya ya Kyerwa zinafanyika katika Maziwa madogo (Sattelite Lakes), Mabwawa na Mto Kagera , Samaki wanaopatikana ni Sato (Tilapia), Kambare (Catfish), na Kamongo (Lung fish).
Taarifa ya mwaka ya Maendeleo ya Mifugo na Uuvi bonyeza TAARIFA YA MWAKA MIFUGO.pdf kusoma zaidi
Kyerwa District Council
Anuani ya Posta: P.O Box 72, KYERWA
Simu ya mezani: +255 686 397 972
Simu ya Mkononi: +255 754 422 746
Barua pepe : ded@kyerwadc.go.tz
Hakimiliki©2017 GWF, Kyerwa District Council. All Rights Reserved